“Zawadi bora ya maisha kwa mwanadamu si fursa ya kufanya kazi kwa bidii na kuwa kitu fulani katika jamii. Ni amani ya Mungu katika moyo wa mwanadamu.”
“Kufanikiwa katika maisha ni kuwa tayari muda wowote kujitoa mhanga kwa ajili ya kitu unachoweza kuwa.”
“Rais wa Tume ya Dunia hakuchaguliwa kuwa kitu katika tume. Alichaguliwa kufanya kitu katika dunia.”
“Watu wanaohatarisha maisha yao kwa kudharau sheria wakati mwingine hawatakiwi kudharauliwa. Ni sawa na mtu aliyepoteza kila kitu katika maisha yake. Wana uwezo wa kufanya chochote.”
“Kujamiiana si anasa tena katika maisha yangu. Ni hitaji muhimu kwa ujenzi wa familia.”
“Nimebadili utaratibu wangu siku hizi kutokana na maadili ya watoto wetu. Siongei na watoto wangu kuhusu Mungu. Naongea na Mungu kuhusu watoto wangu. Yesu alilipa gharama ya maisha yake kutununua kutoka kwa Shetani. Tumrudie; hususan katika kipindi hiki ambacho dunia imekata tamaa.”
“Ukiishi Mexico City katika daraja la watu wakubwa na wewe na anasa ni marafiki wakubwa, hutapenda kuendesha gari ambayo kila mtu anaendesha mjini. Nunua gari na kuibadilisha kuwa ya kwako. Lisa aliponunua gari yake huko Ejército Nacional Mexicano, Mexico City, katika duka la Ferrari, aliipeleka Los Angeles kwa marekebisho aliyoyataka. Ferrari haikuwa ya kawaida. Mbali na kinga ya risasi ya inchi nne, Ferrari ya Lisa ilikuwa na mwendo mkali na matairi makubwa kuliko Ferrari za kawaida. Ilikuwa na rangi tatu: nyeusi, pinki na njano zilizokuwa zikibadilika kulingana na hali ya hewa; na kadhalika ilikuwa na breki ya upepo kwa nyuma, katika buti ya aluminiamu, kwa ajili ya kuikandamiza chini wakati wa mwendo mkali, ili isiyumbe sana barabarani. Lisa peke yake ndiye aliyekuwa na gari ya namna hiyo Mexico City nzima.”